Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Yasin Musawi, Imamu wa Ijumaa wa Baghdad na mwalimu mashuhuri wa Hawza ya Najaf Ashraf, alisisitiza kuwa; kuondoka hatua kwa hatua majeshi ya Marekani na muungano wa kimataifa kutoka Iraq, ni matokeo ya shinikizo la wananchi, bunge na muqawama, na wala si matakwa ya Washington.
Yeye katika hotuba za Ijumaa za wiki hii Baghdad alieleza kwamba majeshi ya Marekani hayakuwa na nafasi yoyote katika kuilinda Iraq, bali walikuwa wakijihusisha tu na kulinda maslahi ya utawala wa Kizayuni, kwa mujibu wake, sehemu ya majeshi yaliyotoka yameelekea mashariki mwa Syria, na sehemu nyingine yamepiga kambi Erbil, mahali ambapo ushawishi wa Israel katika ngazi za kiusalama, kijasusi na kiuchumi ni wa wazi.
Imamu wa Ijumaa Baghdad, akijibu tetesi kuhusu uwezekano wa shambulio la Israel dhidi ya Iraq au Hashd al-Shaabi, alibainisha kuwa: “Hakutakuwa na shambulio lolote, vitisho hivi havina uwezo wowote wa kuleta wasiwasi kwa wananchi wa Iraq, Wazayuni leo hawawezi kuingia katika mpambano wa aina hiyo,” Akiashiria kuwa taarifa zake katika uwanja huu ni za yakini, aliongeza kusema: “Kila uvamizi unaoweza kutokea dhidi ya Iraq hautabaki bila jibu, kama ambavyo ndugu zetu nchini Iran wametilia mkazo, kila pigo dhidi ya Iraq litaambatana na sisi kuingia uwanjani, na Wazayuni ni waoga mno kuingia katika mapambano kama hayo.”
Ayatullah Musawi katika sehemu nyingine ya hotuba yake aligusia uamuzi wa hivi karibuni wa Tume Kuu ya Uchaguzi ya Iraq kuhusu kuwakataa mamia ya wagombea, na kusema hatua hiyo imetokana na kesi za kisheria na uhusiano na chama cha Baath, alitaja kurejea kwa baadhi ya sura za Kibaathi katika nyadhifa za juu za kiserikali kuwa moja ya sababu kuu za kushindwa kisiasa na kiutawala nchini humo.
Yeye pia, akirejea kwenye hali ngumu ya wananchi wa Ghaza chini ya mabomu na kuzingirwa na utawala wa Kizayuni, aliita hali hiyo kuwa “msiba usioweza kuelezwa.” Alionya kuhusu juhudi za Benjamin Netanyahu za kuiunganisha Ghaza ndani ya mradi wa “Israel Kubwa.” Aliongeza kuwa ramani zilizochapishwa na kambi za Kizayuni, ambazo zinahusisha sehemu za Iraq na nchi nyingine za Kiarabu, zinaonyesha kina cha tishio dhidi ya eneo hili.
Imamu wa Ijumaa Baghdad mwishoni mwa hotuba yake, huku akisisitiza kwamba “silaha za muqawama ndani ya Iraq, Lebanon na Palestina zimethibitisha ufanisi wake,” alitoa wito kwa harakati za kisiasa za Iraq kushikamana na misingi na kutojisalimisha mbele ya mashinikizo na mikataba inayolenga kuendeleza uwepo wa wavamizi.
Maoni yako